Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imesaini mkataba wa miezi 18 wenye thamani ya Sh milioni 300 na Kampuni ya Usafirishaji ya Karimjee Group, inayotengeneza pikipiki za Hero.
Akizungumza Alhamisi hii kwenye hafla ya kutiliana saini mkataba huo iliyofanyika Makao Makuu ya klabu hiyo, Kariakoo, Dar es Salaam, Rais wa Yanga, Hersi Saidi alisema makubaliano hayo yanawapa fursa kutangaza bidhaa hiyo ndani na nje ya Tanzania.
Hersi alisema kwamba klabu ya Yanga inanufaika mara mbili katika mkataba huo, moja ni kiasi hicho cha fedha na mbili kupata kamisheni katika kila pikipiki itakayouzwa kupitia kwao.
“Nitoe wito kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga, sasa hivi chapa yetu ya pikipiki kuanzia sasa ni Hero, ukiwa Mwanayanga pikipiki ya kupanda ni Hero, ukiwa dereva wa bodaboda pikipiki sahihi itakayoleta maslahi kwenye klabu yako ni Hero.
“Lakini pia ni bidhaa bora kabisa kutoka kwa kampuni kubwa ulimwenguni ya Hero, pikipiki hiyo pia itakwenda kukufanya wewe Mwanayanga uwe sehemu ya kuchangia maendeleo ya klabu yako lakini pia kuchangia tawi lako,” alisema Hersi.
Alisema watatengeneza kituo maalumu ambacho kitakuwa kinapokea oda za uuzaji wa pikipiki hizo na kitakuwa kinapokea mahitaji ya wanachama kupitia matawi na baada ya kupokea mahitaji hayo, tawi linatakiwa litaje jina la mteja anayetaka kununua na baada ya hapo tawi hilo litakuwa limeorodheshwa kupata kamisheni itakayowanufaisha.
Kwa upande wake, mkuu wa masoko kutoka Karimjee Group, Nada Vievi alisema pikipiki hizo zitakuja na bima kwa mteja pamoja na kofia mbili zenye nembo za Yanga.
