Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amekataa kumhusisha mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe na matokeo ya sare ya bao 1-1 ambayo timu hiyo imeyapata mbele ya Rayo Vallecano.
Real Madrid inayoshika usukani katika Ligi Kuu Hispania au La Liga, sare hiyo imefanya tofauti yake na Girona inayoshika nafasi ya pili kuwa pointi sita huku Real Madrid ikiwa mbele kwa mchezo mmoja.
Katika mchezo huo, Real Madrid iliyokuwa ugenini ilikuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya tatu lililofungwa na Joselu na Vallecano kusawazisha dakika ya 27 kwa penalti iliyotiwa kimiani na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Raul de Tomas.
Baada ya mechi hiyo, Ancelotti aliulizwa iwapo habari ya usajili wa Mbappe Real Madrid ilichangia kuivuruga timu yake na kusababisha matokeo hayo kwa kuwafanya wachezaji wakose umakini, kocha huyo alijibu kwa kuhoji, “Ni lini hasa tumeanza kukosa umakini?”
“Tulianza mechi vizuri na kufunga bao la mapema, baada ya Rayo kupata penalti mchezo ulibadilika, ushindani ulizidi, ilikuwa ni kupambana zaidi na mechi kusimama mara kwa mara, ni matokeo ya sare ambayo hatuyafurahii lakini tutaendelea kupambana, tumejiweka pazuri,” alisema Ancelotti.
“Tunatakiwa kushinda kila mechi lakini ili ushinde taji la ligi ni muhimu pale unapokosa ushindi usipoteze kabisa mchezo, kuna wakati sare inaumiza lakini kwa upande mwingine inaweza kuwa ni hatua nzuri ya kutuwezesha kubeba taji la ligi,” alisema Ancelotti.
Katika mechi hiyo, Real Madrid pia ilipata pigo baada ya mchezaji wake Carvajal kulimwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi kwa kumchezea rafu, Eduardo Camavinga.
Matokeo ya mechi za La Liga jana Jumapili
Rayo Vallecano 1-1 Real Madrid
Granada 1-1 AlmerÃa
Mallorca 1-2 Real Sociedad
Real Betis 0-0 Alaves
