Na mwandishi wetu
Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Saidi amelipongeza benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa timu hiyo kwa kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu NBC wakiwa vinara.
Mabingwa hao watetezi wa ligi wamekamilisha mzunguko wa kwanza kwa kukusanya pointi 40 walizozipata katika michezo 15 ambapo kati ya hiyo wameshinda mechi 13, sare mechi mmoja na kufungwa mara moja.
Akizungumza Dar es Salaam Jumatano hii, Hersi alisema matokeo hayo yametokana na uwekezaji mkubwa walioufanya kwenye kikosi chao ikiwemo kusajili wachezaji wenye ubora na viwango vya kimataifa.
“Mimi na viongozi wenzangu tunalipongeza benchi la ufundi chini ya kocha kuu Miguel Gamondi na wasaidizi wake lakini siwezi kuwasahau wachezaji ambao ndio watendaji wakuu, ukweli tunaona kazi yao na sisi kama uongozi tutaendelea kuwatengenezea mazingira mazuri ili watimize malengo,” alisema Hersi.
Kiongozi huyo alisema wamekuwa karibu na timu yao lengo likiwa ni kuendeleza mafanikio waliyoyapata kwenye misimu miwili iliyopita walipobeba mataji yote ya ndani na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Alisema mikakati yao ni kuongeza kasi ya kupata matokeo mazuri kwenye mzunguko wa pili na kubeba taji hilo kwa mara ya tatu na kwa mwendo walionao anaamini hilo linaweza kutimia pasipo na shaka yoyote.
Kutokana na msimamo wa ligi ulivyo hivi sasa, Yanga inahitaji kushinda idadi kama hiyo ya mechi kwenye mzunguko wa pili ili kutetea taji hilo kwa msimu wa tatu mfululizo.
