Na mwandishi wetu
Kikosi cha Yanga leo Jumanne kimeanza maandalizi ya kuikabili CR Belouizdad katika mchezo wa tano wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Februari 24, mwaka huu.
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D, sawa na vinara Al Ahly, lakini mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa wana mchezo mmoja mkononi dhidi ya Belouzidad yenye pointi tatu utakaochezwa Algeria, Februari 16, mwaka huu.
Kuelekea mchezo huo meneja wa Yanga, Walter Harrison alisema wameamua kuanza maandalizi mapema lengo likiwa ni kushinda mchezo huo na kujiweka katika mazingira mazuri ya kwenda hatua ya robo fainali.
“Huu ni mchezo muhimu sana ambao kama tutashinda itakuwa tuna asilimia kubwa ya kutinga robo fainali bila kuangalia matokeo ya timu nyingine, ndio maana viongozi wa timu pamoja na benchi la ufundi wameanza mikakati ya ushindi mapema,” alisema Walter.
Meneja huyo alisema kwa sasa timu hiyo itakuwa inafanya mazoezi mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni na watakuwa wanatokea nyumbani na wanatarajia kuingia kambini ikibaki wiki moja kabla ya mchezo huo.
Katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa ilizocheza Yanga mpaka sasa, timu hiyo imeshinda mchezo mmoja, imetoka sare michezo miwili na kufungwa mara moja.
