Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid imethibitisha kuwa kiungo wake, Jude Bellingham atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu baada ya kuumia enka katika mechi ya La Liga dhidi ya Girona iliyochezwa Jumamosi.
Katika mechi hiyo ambayo Real Madrid ilitoka na ushindi wa mabao 4-0, Bellingham alifunga mawili kati ya hayo na kuifanya timu yake iongoze ligi ikiwa imeizidi Girona inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tano.
Bellingham alilazimika kutoka nje kabla ya mpira kumalizika ambapo kocha wake, Carlo Ancelloti alinukuliwa baada ya mechi akisema kwamba mchezaji huyo atafanyiwa vipimo kabla ya kuthibitishwa kwamba atakuwa nje wiki tatu.
Kuumia kwa mchezaji huyo kumekuja wakati mbaya kutokana na ratiba ngumu ya timu hiyo ambayo kesho Jumanne itakuwa uwanjani katika mechi ya hatua ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RB Leipzig ya Ujerumani.
Real Madrid pia mwishoni mwa wiki itakuwa uwanjani kusaka pointi nyingine tatu muhimu za kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa La Liga itakapoumana na Rayo Vallecano.
Bellingham ambaye huu ni msimu wake wa kwanza na Real Madrid, ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa hadi sasa amezifumania nyavu mara 20 katika mashindao yote huku mabao 16 kati ya hayo akiyafunga kwenye La Liga.
Kimataifa Bellingham nje wiki tatu
Bellingham nje wiki tatu
Read also
