Barcelona, Hispania
Kiungo wa zamani wa Real Madrid, Guti (pichani) anaamini Xavi hakuwa amejiandaa kuinoa Barcelona na amepewa timu hiyo katika wakati ambao si sahihi.
Xavi, kiungo wa zamani wa Barca, hivi karibuni ametangaza kwamba atang’atuka kuinoa timu hiyo baada ya msimu huu kwa kinachoaminika kuwa hafurahishwi na mambo yanavyokwenda na amewahi kusema kwamba hathaminiwi.
Kocha huyo alianza kuinoa Barca mwaka 2021 akitokea klabu ya Al-Sadd ya Qatar na mwaka 2023 aliiwezesha kubeba taji la La Liga pamoja na lile la Spanish Super Cup.
Kwa sasa Barca inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga ikiwa na pointi 50, tofauti ya pointi nane dhidi ya vinara wa ligi hiyo Real Madrid na sita dhidi ya Gerona inayoshika nafasi ya pili.
“Xavi Hernandez hakujiandaa kuja kuinoa Barcelona, alidhani kwamba kila kitu kingekuwa rahisi lakini hapana, unapokuwa Qatar na kuiandaa timu mbele kukiwa na mashabiki 300, hiyo si sawa na kuwa kwenye benchi la Barcelona, huo ndio ukweli,” alisema Guti ambaye amewahi kunukuliwa akidai kwamba ana ndoto ya kuinoa Real Madrid miaka ijayo.
Xavi ameichezea Barca kwa miaka 17 na kucheza jumla ya mechi 767 na kushinda mataji 25, hata hivyo amesema kwamba hafuti moja kwa moja uwezekano wa yeye kurudi kwa mara nyingine kuinoa Barca hapo baadaye.
Kimataifa Guti: Xavi hakujiandaa kuinoa Barca
Guti: Xavi hakujiandaa kuinoa Barca
Read also
