Timu ya Azam FC inatarajia kuondoka Dar es Salaam leo Alhamisi kuelekea Mwanza kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Simba SC.
Akizungumza na GreenSports, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Youssouf Dabo alisema katika safari hiyo atawajumuisha nyota wake wote lengo likiwa ni kuvuna pointi tatu zitakazowarudisha kileleni mwa msimamo wa ligi.
“Tunakwenda Mwanza tukiwa na kikosi kamili sababu huu ni mchezo mkubwa na lengo letu ni kushinda, tunafahamu wapinzani wetu si timu ya kubeza, wana kikosi kizuri pamoja na benchi zuri la ufundi kwa hiyo tumejipanga kuhakikisha tunacheza soka la kuvutia na kuvuna pointi tatu,” alisema Dabo.
Alisema kwa namna alivyokiandaa kikosi chake haofii mchezo huo kupelekwa Mwanza kwani ubora na muunganiko waliokuwa nao popote wanaweza kucheza na kupata ushindi bila kujali wanacheza na timu gani.
“Kipindi ambacho ligi ilisimama sisi tulijikita zaidi kwenye maandalizi ya ligi yote, si kwa ajili ya Simba tu na tulicheza mechi nyingi za kirafiki na timu za Zanzibar ambazo naamini zilikuwa ni kipimo kizuri kwa ajili ya kuwaweka tayari wachezaji kuelekea mechi za ligi na za Kombe la FA,” alisema Dabo.
Azam kwa sasa ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu NBC ikikusanya pointi 31, pointi tatu nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 34 baada ya kila timu kucheza mechi 13.
