Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ameelezea hofu yake ya kupoteza namba baada ya kuumia bega katika mchezo wa Ligi Kuu NBC uliopita dhidi ya Kagera Sugar.
Akizungumza na GreenSports, mchezaji huyo alisema ushindani mkubwa wa namba uliopo kwenye kikosi chao ndicho kinachompa hofu juu ya kuendelea kupigania namba.
“Hofu yangu ni kwamba nikipona nafasi yangu itakuwa imechukuliwa na mtu mwingine na mimi nitalazimika kuanza upya kuirudisha na unajua Yanga kila mchezaji ni bora na anapambana kucheza kikosi cha kwanza,”alisema Sure Boy.
Kwa upande wake daktari wa Yanga, Moses Etutu, alisema mchezaji huyo alipata mshtuko kwenye bega lake la kulia na baada ya kumpatia tiba ya haraka anaendelea vizuri.
Alisema kutokana na maumivu aliyoyapata mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki mbili hadi tatu kabla ya kurejea uwanjani kwa mara nyingine.
Katika kikosi cha Yanga, kiungo huyo wa zamani wa Azam FC, anawania namba na Mudathir Yahya na Khalid Aucho ambao wamekuwa chaguo la kwanza la kocha Miguel Gamondi raia wa Argentina.
