Berlin, Ujerumani
Uamuzi wa kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp kutangaza kuachana na timu hiyo baada ya msimu huu umepokewa vizuri na baadhi ya mashabiki wa soka Ujerumani wakiamini ndiye mtu sahihi kukabidhiwa timu yao ya taifa.
Mtazamo huo unabebwa na mwenendo usio mzuri wa timu ya taifa ya Ujerumani kuanzia kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022 ambapo timu hiyo yenye heshima yake katika soka duniani iliaga fainali hizo mapema.
Uamuzi wa Klopp umeshangaza kwani umekuja wakati Liverpool ikionekana kuwa imara zaidi katika mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu England (EPL) ikiwa ndiyo timu inayoshika usukani.
Hiyo ni baada ya kupitia kipindi cha msukosuko wa matokeo yasiyoridhisha lakini alivumilia na ajabu mambo yameanza kunyooka lakini kocha huyo ameamua kuja na uamuzi huo mgumu na ulioshangaza wengi.
Kiujumla Klopp ni kocha ambaye ameipa mafanikio makubwa Liverpool kuanzia kuipa taji la EPL, kuifikisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na safari hii ilitarajiwa angefikia hatua hiyo au hata kubeba mataji hayo mawili makubwa.
Mafanikio ya Liverpool chini ya Klopp ni mambo ambayo Wajerumani wamekuwa wakiyakosa kwenye timu yao ya taifa na katika hali ya kawaida kwa makocha wengi Wajerumani, jina la Klopp linaweza kuwa namba moja kati ya majina yanayofaa kukabidhwa kikosi cha Ujerumani.
Mashabiki Ujerumani wanadhani ni wakati sahihi kwa kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund kuyahamishia mafanikio yaliyoonekana Liverpool kwenye timu ya taifa lake.
Hadithi ya Klopp kuhusishwa na timu ya taifa ya Ujerumani haijaanza sasa, ilikuwa hivyo Septemba mwaka jana baada ya Hansi Flick kutimuliwa kuinoa timu ya taifa.
Chama cha Soka Ujerumani (DFB) kiliamua kumkabidhi timu hiyo, Julian Nagelsmann, kocha wa zamani wa klabu za Bayern Munich na RB Leipzig ambaye pia baadhi ya mashabiki hawakuridhishwa na uteuzi wake.
Nagelsmann ambaye pia mwenendo wake na timu hiyo si wa kuridhisha, amesaini mkataba ambao utafikia ukomo baada ya fainali za Kombe la Ulaya 2024 (Euro 24) ambazo zitafanyika nchini Ujerumani kuanzia Juni mwaka huu.
Klopp ameshasema kwamba hatofundisha timu yoyote ya England zaidi ya Liverpool, na hapo ndipo swali linapokuja je atakwenda timu gani baada ya kuachana na Liverpool kama si timu yake ya taifa?
Kimataifa Klopp asubiriwa timu ya taifa Ujerumani
Klopp asubiriwa timu ya taifa Ujerumani
Read also
