Liverpool, England
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya Misri, Mohamed Salah ameanza tiba ya majeraha ya misuli ya nyuma ya goti huku akiahidi kufanya kila linalowezekana ili arudi Ivory Coast kuiwakilisha Misri kwenye fainali za Afcon.
Salah alilazimika kurudi Liverpool Jumatano iliyopita kwa ajili ya tiba ya majeraha aliyoyapata wiki iliyopita wakati akiiwakilisha Misri dhidi ya Ghana kwenye mechi ya Afcon hatua ya makundi, mechi iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
“Jana (juzi) nilianza utaratibu wa kupata matibabu na mazoezi ya kujiweka sawa, na nitafanya kila niwezalo ili nipone haraka iwezekanavyo na kurudi kwenye timu ya taifa kama tulivyokubaliana mwanzo,” aliandika Salah kupitia mitandao ya kijamii.
Kocha mkuu wa Liverpool, Jurgen Klopp pia alisema anaamini Salah atarudi kwenye fainali za Afcon kama atapona kwa wakati majeraha yanayomkabili na iwapo Misri itafikia hatua ya fainali.
Naye kocha msaidizi wa Liverpool, Pepijn Lijnders alisema Salah anatarajia kurudi uwanjani kwa kipindi cha wiki mbili au tatu kama hakutakuwa ni kitu cha kumkwaza katika tiba anayoendelea kuipata.
Kwa mujibu wa Lijnders uamuazi wa kumtaka Salah akapatiwe matibabu Liverpool haukuwa na lengo la kumuondoa kwenye timu ya Misri bali ni kuhakikisha anapata matibabu bora na sahihi.
Wakati huo huo, Klopp aliwajia juu wachambuzi na wanasoka wa zamani waliodai kwamba Salah ambaye pia ni mshambuliaji tegemeo wa Liverpool, alitakiwa kubaki Ivory Coast na kikosi cha Misri.
“Kama kuna watu wanahoji uadilifu wa Mo Salah wanatakiwa wajiulize kama uadilifu wao upo sahihi kwa sababu Mo Salah ni mchezaji muadilifu zaidi kwa timu yake ya taifa kati ya wachezaji niliowahi kukutana nao katika maisha yangu,” alisema Klopp.
Wakati mjadala wa Misri kumtumia au kutomtumia Salah kwenye Afcon ukiwa umepamba moto, Misri kwanza italazimika kufuzu mtihani wa Jumapili dhidi ya DR Congo katika mechi ya mtoano au 16 bora.
