Na mwandishi wetu
Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema kuelekea mechi ya kesho Jumatano dhidi ya DR Congo, watapambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Samatta amesema hayo leo Jumanne alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nchini Ivory Coast kuelekea mechi yao ya kesho Jumatano ya kumaliza hatua ya makundi ya michuano ya Afcon.
Alisema ingawa wachezaji wana majonzi na masikitiko kwa kupata sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita dhidi ya Zambia waliokuwa na kadi nyekundu lakini wanajitahidi kuwekana sawa wakifahamu wanahitaji kupata matokeo kesho.
“Nadhani mechi ya mwisho ya Zambia imewapa wachezaji wengi masikitiko, wengi waliamini tutapata ushindi lakini mwisho haikuwa hivyo, sasa tunajaribu kuzungumza na kurudishana katika hali ya mchezo ili tuhakikishe mchezo wa kesho tunakuwa bora.
“Sababu kama tuliweza kuamini tunaweza kupata ushindi na Zambia basi inawezekana tukafanya hivyo kwenye mechi na DR Congo.
“Wachezaji wote wanaelewa umuhimu wa mchezo wa kesho na nini tunapaswa kufanya hivyo tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Samatta.
Stars inaingia dimbani ikiwa inaburuza mkia katika Kundi F ikiwa na pointi moja, ikihitaji ushindi ili ifikishe pointi nne huku ikiiombea mabaya Zambia ifungwe na Morocco katika mchezo wao wa mwisho ili isonge hatua ya mtoano ya michuano hiyo.
Morocco ndio kinara ikiwa na pointi nne baada ya ushindi wa mabao 3-0 kwa Stars na sare ya bao 1-1 dhidi ya DR Congo inayoshika nafasi ya pili kwa pointi mbili, sawa na Zambia inayoshika nafasi ya tatu.
