Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema kitendo cha kupoteza umakini kimewagharimu na kushindwa kuondoka na pointi tatu na kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia.
Katika mchezo huo wa Kundi F uliochezwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Laurent Pokou, San Pedro, Stars walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 11 lililofungwa na Simon Msuva huku Patson Daka akiisawazishia Zambia dakika ya 89.
“Ilikuwa mechi ngumu tuliuanza mchezo vizuri kwa kujaribu kuwakabia juu na tukafanikiwa kupata bao la haraka kwenye robo ya kwanza ya mchezo na tukafanikiwa kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza salama.
“Naijua timu hii tuliwafuatilia vizuri, kwenye mchezo wa mpira wa miguu timu yenye wachezaji 10 uwanjani ni hatari kwani tulipoteza umakini kitu kilichotugharimu tukaruhusu bao dakika za mwisho,” alisema Morocco.
Tanzania yenye pointi moja mkiani imebakiza mchezo mmoja kwenye hatua ya makundi, wakihitaji ushindi mechi ya mwisho dhidi ya DR Congo kuwania nafasi ya kutinga hatua ya mtoano.
“Tuliingia kwenye mchezo huu kusaka pointi tatu lakini tumeondoka uwanjani na pointi moja ndio mpira. Tuna timu changa ambayo inaendelea kujifunza kila baada ya mchezo kuna baadhi ya wachezaji hawakuwa fiti, tunalifanyia kazi hilo naamini kwenye mchezo ujao tutakuwa bora,” aliongeza Morocco.
Kocha wa Zambia Avram Grant: “Ni matokeo yenye kufadhaisha. Tulijua haitakuwa mechi rahisi baada ya kuona mchezo wa Tanzania dhidi ya Morocco. Ni kweli sisi pia tulianza vizuri lakini tulikubali bao haraka na hiyo ilibadilisha mbinu zetu, hasa baada ya kadi nyekundu.
“Ni ngumu kucheza na wachezaji 10 lakini nafurahia mwamko wa vijana wangu walijitoa kwa kila kitu,” alisema Grant.
Morocco, waliotinga nusu fainali ya Kombe la Dunia huko Qatar mwaka 2022, watakuwa kibarua kikubwa kwa wachezaji wa Grant.
Zambia itakayoumana na Morocco mchezo wa mwisho wa makundi, inashikilia nafasi ya tatu kwa pointi mbili, sawa na DR Congo. Morocco inaongoza kundi kwa pointi nne.
