Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amewashauri mashabiki wa timu hiyo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wao na kuacha kusikiliza watu wachache wasioitakia mema timu yao.
Baadhi ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameoneshwa kutoridhishwa na utendaji wa kiongozi huyo ikiwemo ishu za usajili na mwenendo wa timu yao katika mashindano wanayoshiriki.
“Tuache kusikiliza watu wachache ambao hawana nia njema na timu yetu, lawama zimekuwa nyingi kuhusu viongozi na mbaya zaidi maneno haya yanakuja timu inapopata matokeo mabaya katika baadhi ya mechi tu.
“Ndugu zangu huko ni kutowatendea haki viongozi wenu ambao tunahangaika usiku na mchana kuleta furaha katika timu kwa ujumla,” alisema Mangungu.
Alisema pamoja na chuki hizo, yeye na wenzake wapo imara na wataendelea kuiongoza Simba kwa kufuata sheria na kanuni za katiba ya Simba ili kufika malengo wanayoyakusudia ambayo ni kuifanya timu hiyo kuwa bora na yenye mafanikio Afrika.
Mangungu alirejea madarakani awamu ya pili, Januari 29, mwaka jana na anatarajiwa kukaa madarakani hadi Januari 2026 kipindi ambacho uongozi wake utafikia ukomo.
