Abidjan, Ivory Coast
Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah ataondoka kwenye kambi ya timu yake ya taifa nchini Ivory Coast na kwenda Liverpool kupata tiba ya matatizo ya misuli yanayomkabili.
Salah yuko Ivory Coast akiiwakilisha timu ya taifa ya Misri kwenye fainali za Afcon na leo Jumatatu timu yake itacheza na Cape Verde na inadaiwa mchezaji huyo atakuwa jukwaani wakati wa mechi hiyo.
Chama cha Soka Misri (Efa) kimethibitisha kuwa Salah ataendelea na matibabu katika klabu yake ya Liverpool kama ilivyoshauriwa na kocha Jurgen Klopp jana Jumapili baada ya mechi ya Liverpool na Bournemouth katika Ligi Kuu England, mechi ambayo Liverpool ilishinda kwa mabao 4-0.
“Matumaini yetu ni kwamba tutakuwa naye katika hatua ya nusu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kama tutafuzu hatua hiyo,” ilieleza taarifa ya Efa.
Salah aliumia Alhamisi iliyopita katika mechi dhidi ya Ghana iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2 na hadi sasa haijawekwa wazi muda ambao majeraha yaliyompata yatapona.
Alipokutana na waandishi wa habari juzi Jumamosi, Salah hata hivyo alikwepa kuzungumzia hali ya majeraha yanayomkabili na anatarajia lini kupona.
Klopp alinukuliwa mara baada ya Salah kuumia akisema kwamba anatarajia mchezaji huyo atarudi Liverpool kwa ajili ya tiba au walau kupata wasaa wa kuwa pamoja na timu ya madaktari wa klabu hiyo.
