Na mwandishi wetu
Mkutano mkuu wa klabu ya Simba uliofanyika leo Jumapili jijini Dar es Salaam, umetangaza bajeti ya Sh 25 bilioni kwa msimu wa 2023-24 ikiwa ni ongezeko la takriban Sh 10 bilioni kulinganisha na bajeti iliyopita.
Kwa mujibu wa mhasibu wa klabu hiyo, Seleman Kahumbu, bajeti hiyo itategemea vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwamo udhamini, mapato ya viingilio vya mechi, haki za matangazo, uuzaji wa jezi na udhamini mkubwa na mdogo.
Kahumbu pia aliwaarifu wanachama kuwa mwekezaji na rais wa heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji au Mo Dewji amekuwa nao pamoja katika kuifanikisha bajeti hiyo na kutolea mfano msimu uliopita ambao alichangia Sh 2.4 bilioni.
Wanachama wa klabu hiyo pia wamepitisha baadhi ya vipengele vya maboresho ya katiba yao kwa lengo la kutimiza matakwa ya serikali.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya maboresho ya katiba ya Simba, Hussein Kitta, wanachama hao wamepitisha mambo sita ingawa suala lililokuwa likisubiriwa kwa hamu la uwakilishi wa wanachama kwenye mkutano mkuu liligonga mwamba.
Wanachama wa Simba kwa pamoja wamekipinga kipengele kilichokuwa kikipendekeza kupunguza idadi ya uwakilishi wao kwenye mkutano mkuu na kutaka uwakilishi uwe wa watu wachache kutoka kila tawi la klabu hiyo.
Mgeni rasmi katika mkutano huo, Nicolas Mihayo ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), aliwapongeza wanachama wa Simba kwa kufuata maelekezo waliyopewa na serikali na kuzitaka klabu nyingine kuiga mfano huo.
Soka Mkutano Simba watangaza bajeti ya bilioni 25
Mkutano Simba watangaza bajeti ya bilioni 25
Read also
