Na mwandishi wetu
Beki wa kati wa Simba, Che Fondoh Malone anaamini Taifa Stars itazifunga Zambia na DR Congo na kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) inayoendelea nchini Ivory Coast.
Taifa Stars imeanza vibaya michuano hiyo baada ya jana Jumatano kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa timu ya taifa ya Morocco.
Mlinzi huyo raia wa Cameroon ameiambia GeeenSports kuwa Tanzania ilicheza vizuri na kuwadhibiti Morocco isipokuwa makosa madogo na kadi nyekundu ya kipindi cha pili ndivyo vilivyochangia wapoteze mchezo huo.
“Nimeangalia mechi zote mbili za Kundi F, nilichobaini Tanzania inaweza kuzifunga Zambia na Congo na kutinga hatua ya 16 bora, sababu walicheza vizuri na makosa madogo na kadi nyekundu ndiyo vilichangia wapoteze mchezo,” alisema Che Malone.
Alisema kingine ambacho kilisababisha Stars wapoteze mchezo huo ni presha waliyokuwa nayo wachezaji ambayo ilitokana na kuanza na timu kubwa lakini anaamini hilo halitokuwepo kwenye mechi mbili zinazofuata.
Beki huyo pia aliizungumzia timu yake ya Cameroon akisema licha ya kuanza kwa sare dhidi ya Guinea lakini wanayo nafasi ya kufika mbali kutokana na ubora wa kikosi walichonacho.
