Na mwandishi wetu
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) litakuwa mubashara kwa kuonesha mechi 52 na kutangaza kwa redio mechi 64 za michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) itakayofanyika Ivory Coast kwa ubora.
Michuano hiyo itaanza rasmi Januari 13 hadi Februari 11, mwaka huu ambapo mashabiki wa soka nchini watapata fursa ya kushuhudia mitanange hiyo kupitia TBC 1, TBC 2, TBC Taifa, na TBC Online.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne hii, Mkurugenzi wa TBC, Dk Ayub Rioba alisema mwaka huu wanawaletea Watanzania matangazo ya mataifa ya Afrika kwa kiwango cha HD yaani picha inaonekana kama uko uwanjani.
“Mwaka huu shirika limepata haki ya kurusha matangazo ya michuano ya Afcon, kwa njia ya televisheni na redio na mitandao ya kijamii, niwataarifu Watanzania wenzangu kuwa maboresho makubwa tumefanya kama ilivyokuwa kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022,” alisema Dk Rioba.
Alisema mwaka 2022 kulikuwa na tatizo la kukatika kwa matangazo kwa asilimia ndogo lakini mwaka huu tatizo hilo halitokuwapo kwani kuna chaneli nyingine kama ile safari itaendelea kutumika ili kutokwamisha jambo hili.
“Tunaomba mpokee matangazo hayo kutoka TBC na tunafahamika kwa umahiri wetu wa kuwa na wachambuzi na watangazaji bora hilo liko wazi,” alisema Rioba.
Wakati huo huo, Rioba alisema inafahamika TBC inapatikana kwenye visimbusi vyote kwa sababu ni lazima ipatikane iwe mtu amelipia, hajalipia lazima aione hivyo ni fursa kwa Watanzania kujionea burudani hii.
“Tunawaomba wadhamini wanaotaka kutangaza nasi hii sio fursa ya kukosa ili waweze kuona ubora ambao TBC inafahamika nchi nzima.,” alisema Rioba.
