Rio de Janeiro, Brazil
Shirikisho la Soka Brazil (CBF) hatimaye limeamua kuachana na kocha wa muda wa timu ya taifa, Fernando Diniz (pichani) na sasa linamsaka kocha ambaye atakuwa wa kudumu.
Diniz ambaye ana mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo ameiongoza katika mechi sita za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 na kati ya hizo amepoteza tatu, kashinda mbili na sare moja.
Akiwa na timu ya Brazil, Diniz pia ameendelea na kibarua chake cha kuinoa timu ya Fluminense ambao kwa sasa ndio mabingwa wa Copa Libertadores jambo ambalo inadaiwa mabosi CBF hawalifurahii.
“CBF tunamshukuru Fernando Diniz kwa kazi aliyoifanya na kwa namna alivyojitolea na umakini aliouonesha na kwa changamoto za kuiweka sawa timu ya Brazil wakati wa kipindi chake, tunamtakia kila la kheri,” ilieleza taarifa ya CBF.
Rais wa CBF, Ednaldo Rodrigues, juzi Alhamisi alizungumza na rais wa klabu ya Fluminense, Mario Bittencourt kuhusu mpango wa kuajiri kocha wa kudumu kwa maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo zitafanyika katika nchi za Canada, Mexico na Marekani.
Brazil imekuwa bila ya kocha wa kudumu tangu Tite ang’atuke katika nafasi hiyo baada ya timu hiyo kufungwa na Croatia na kutolewa katika hatua ya robo fainali ya fainali za Kombe la Dunia 2022.
Baada ya Tite kujiuzulu, kocha wa timu ya Brazil ya vijana chini ya miaka 20, Ramon Menezes alikabidhiwa jukumu hilo kwa muda kabla ya kuteuliwa kwa Diniz.
Julai mwaka jana Rodrigues alisema kwamba kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti angepewa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil jambo ambalo lingemfanya kuwa kocha wa kwanza asiye mzawa kuinoa timu hiyo.
Mpango huo hata hivyo ulizikwa rasmi mwezi uliopita baada ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 64 kusaini mkataba wa miaka miwili na Real Madrid na sasa atakuwa na timu hiyo hadi Juni 2026.
