Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba rasmi imeteuliwa kuwa Balozi wa Utalii wa Zanzibar na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Simai Mohammed Said.
Hafla ndogo ya makubaliano hayo imefanyika leo Ijumaa visiwani Zanzibar ambako Simba inaendelea na mechi za michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Waziri Simai amechukua uamuzi huo kwa kutambua mchango wa klabu hiyo inayoutoa katika kutangaza utalii wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika michuano mbalimbali inayoshiriki ikiwemo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, alisema: “Tunaishukuru sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutambua mchango wa timu yetu kutangaza utalii, hivyo kukuza uchumi wa Zanzibar. Tunaona fahari kubwa kuwa sehemu ya maendeleo makubwa inayoyapata Zanzibar.”
Kabla ya uteuzi huo, Simba ilikuwa ikiendesha kampeni mbalimbali za kuutangaza utalii wa Zanzibar kupitia mashindano ya Mapinduzi ikiwemo kuvaa jezi yenye nembo ya VisitZanzibar katika mechi zote za mashindano hayo lakini pia kupitia mitandao yake ya kijamii.
Pia huu ni takriban msimu wa tano,Wekundu hao wamekuwa wakivaa kifuani nembo ya Visit Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Soka Simba SC Balozi wa utalii Zanzibar
Simba SC Balozi wa utalii Zanzibar
Read also
