Paris, Ufaransa
Baada ya kuhusishwa na klabu za Real Madrid na Liverpool katika siku za karibuni, hatimaye mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe amesema bado hajaamua timu gani atajiunga nayo baada ya msimu huu.
Mbappe ambaye jana Jumatano aliisaidia PSG kuichapa Toulouse mabao 2-0 na kubeba kombe la Ufaransa amesema hadi sasa hajaamua kuhusu hatima yake wakati mkataba wake na PSG ukielekea mwisho.
Mkataba wa Mbappe na PSG unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu wa 2023-24 na kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid ingawa kwa siku za karibuni Liverpool nayo imekuwa ikihusishwa kumtaka mchezaji huyo.
“Awali ya yote nimekuwa mwenye kushawishika kwa sana kwa mwaka huu, hilo ni jambo muhimu,” alisema Mbappe.
Akizungumzia bao alilofunga katika mechi na Toulouse na hatimaye kubeba kombe, Mbappe aliongeza, “Kama nilivyosema tuna mataji tunayoyapigania na tayari tumeshinda moja, kwa hiyo hilo limekwisha, baada ya hilo bado sijaamua lolote.”
“Lakini kwa namna yoyote ile kutokana na makubaliano niliyofanya na mwenyekiti (Nasser Al-Khelaifi) kuhusu majira ya kiangazi, haijalishi nini nitakachoamua,” alisema Mbappe.
“Tumefanikiwa kujali maslahi ya pande zote na kuimarisha utulivu wa klabu kwa ajili ya changamoto zilizo mbele yetu, hilo linabaki kuwa jambo lenye muhimu, hayo mengine ni mambo yanayofuata,” alisema Mbappe.
Mbappe alijiunga na PSG mwaka 2017 kutoka klabu ya Monaco, awali klabu hiyo ilimchukua kwa mkopo kabla ya kumsajili rasmi kwa ada ya Pauni 167 milioni.
