Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amemtaka mchezaji mpya wa timu hiyo Augustine Okrah kuonesha kwa vitendo imani ambayo viongozi na mashabiki wa timu hiyo wanayo juu yake.
Okrah aliyeitumikia Simba msimu uliopita amejiunga na Yanga hivi karibuni kwa mkataba wa miaka miwili akitokea timu ya Bencham United ya kwao Ghana.
Gamondi raia wa Argentina alisema timu yake ilihitaji kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kulingana na ugumu wa mashindano wanayoshiriki na ukubwa wa Yanga hivyo Okrah anapaswa kujituma na kuonesha kwa vitendo kwamba anastahili kucheza timu hiyo.
“Sihitaji kuzungumza mambo mengi kuhusu yeye, kama kocha nitampa nafasi aonyeshe kwa vitendo ubora wake utakaompa nafasi ya kucheza zaidi endapo atashindwa kufanya kile tunachokitarajia kutoka kwake atawapisha wengine wacheze,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema kwa ukubwa na malengo ya Yanga, hivi sasa hawahitaji kumpa muda mchezaji kulingana na aina ya mashindano lakini pia uhitaji wa matokeo kuwa mkubwa katika kila mechi.
Alisema kwenye kikosi chake ana wachezaji wenye uwezo na rekodi nzuri huko walikotoka lakini wameshindwa kuingia mapema kwenye mfumo wa Yanga na yeye ameshindwa kuwatumia sababu ya uhitaji wa matokeo.
Malengo ya Yanga msimu huu ni kufika robo fainali kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea mataji yote ya ndani ambayo ni Ligi Kuu NBC na Kombe la ASFC (FA).
