Na mwandishi wetu Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameeleza namna anavyojivunia mafanikio ya Simba kwa miaka mitano iliyopita na kamwe hawatokubali kurudi nyuma.
Kauli hiyo ya Mo imekuja ikiwa ni siku mbili zimepita tangu timu hiyo itolewe kwenye michuano ya Kombe la Azam (ASFC) kwa kufungwa na Yanga bao 1-0 kwenye hatua ya nusu fainali katika mechi iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kabla ya kutoa kauli hiyo leo Mo ambaye ni rais wa heshima wa klabu hiyo, awali juzi pia alitoa tamko la kupendekeza bodi ya wakurugenzi ya timu hiyo kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kuipeleka timu hiyo kwenye njia iliyo bora na mafanikio zaidi ya ile ya miaka mitano iliyopita.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Mo aliandika: “Kwa ujumla miaka mitano iliyopita imekuwa ya mafanikio kwa Simba. Bajeti iliongezeka mara tano, tulishinda makombe mengi ya ndani na tuliweka alama kimataifa kwa kufika robo fainali tatu za michuano ya Afrika.
“Hii imekuwa mara ya kwanza Simba imekuwa na mwendelezo mzuri katika miaka 86 ya historia yetu. Hakuna kurudi nyuma tunatakiwa kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo tuna madhaifu na kwenda mbele. Mapambano yanaendelea.”
Licha ya kupoteza kwenye nusu fainali hiyo ambayo Simba ilikuwa bingwa mtetezi wa kombe hilo lakini kauli hizo za Mo pia zimechagizwa na Simba kushindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga wamebakiza kuvuna pointi tatu na kuutwaa rasmi.
Kipindi cha miaka mitano aliyoigusia Mo ni kipindi ambacho Simba ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara nne mfululizo na kuitawala ligi kwa kiasi kikubwa ikiwemo pia kufika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili na msimu huu kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutupwa nje na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Msimu huu Simba imefanikiwa kuambulia ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi pekee ilioupata kwa kuifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan. Bao pekee la mechi hiyo liliwekwa kimiani na Meddie Kagere.
Soka Mo: Simba hakuna kurudi nyuma
Mo: Simba hakuna kurudi nyuma
Related posts
Read also
