Eldoret, Kenya
Polisi nchini Kenya wanachunguza maauji ya mwanariadha wa Uganda, Benjamin Kiplagat (pichani) ambaye mwili wake umekutwa ndani ya gari ya kaka yake ukiwa na majeraha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa eneo hilo, Stephen Okal, Kiplagat alikuwa akiendesha gari hilo kabla ya umauti kumkuta katika mji wa Eldoret uliopo maili 160 magharibi wa jiji la Nairobi.
Mwili wa mwanariadha huyo maarufu katika nchi za Kenya na Uganda ulikutwa jana Jumapili ukiwa na majeraha katika tukio ambalo linadhaniwa kuwa ni mpango maalum ulioandaliwa kwa lengo la kumtoa uhai mwanariadha huyo.
“Haya ni mauaji lakini kwa sasa bado hatujajua nini hasa kimesababisha mauaji haya,” alisema kamanda Okal.
Kiplagat alikuwa akikimbia zaidi mbio za mita 3,000, amewahi kuiwakilisha Uganda katika mashindano ya dunia mara sita, kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Kiangazi mwaka 2008, 2012, 2016 na katika Michezo ya Olimpiki London ya 2012 alifikia hatua ya nusu fainali.
Kifo cha Kiplagat kimezua taharuki nchini Kenya na Uganda hasa kwa kuwa imekuwa vigumu kujua nini hasa sababu ya mauaji hayo ya kikatili.
