Na mwandishi wetu
Kocha Msaizidi wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Hemed Morocco amesema wanaridhishwa na ushindani uliopo katika mazoezi ya timu hiyo, kila mmoja akionesha yupo tayari kupata nafasi ya kuipigania timu hiyo.
Morocco amezungumza hayo leo Jumamosi akifafanua kuwa kwa mazoezi waliyofanya siku mbili mfululizo kwa vipindi vinne kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar imeleta faraja na kuonesha mwanzo mzuri wa maandalizi ya michuano ya Afcon, Januari, mwakani.
Alisema kuwa wachezaji hao wamekuwa vizuri kimaandalizi kuanzia kwenye fiziki na kiakili na kuibua ari mpya ndani ya kikosi hicho.
“Tunashukuru Mungu tupo na afya njema, kifiziki na kiakili wachezaji wote wako kwenye kiwango kizuri, ni mazoezi mazuri ndani ya siku mbili hizi kwa vipindi vinne tofauti na hata mechi tuliyocheza (Kilimajaro dhidi ya Zanzibar) imetuonesha pa kuanzia.
“Vilevile pia kila mchezaji aliyepo hapa ameonesha anataka kupata nafasi ya kuipambania timu, kwa hiyo ni kitu cha faraja kwetu na tumekuwa na maendeleo mazuri, ambalo nalo ni jambo jema mno kwetu,” alisema Morocco.
Stars inatarajia kwenda kuweka kambi ya mwisho nchini Misri hivi karibuni kabla ya kuelekea Ivory Coast inakofanyika michuano hiyo na karata yake ya kwanza ikitarajia kuumana na Morocco, Januari 17, mwakani.
