Paris, Ufaransa
Wenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 wameahidi kuifanya michezo hiyo kuwa ya mfano wa kipekee katika kuhakikisha haihusishi uharibifu wa mazingira ikiwamo kupunguza kiwango cha hewa ukaa kwa asilimia 50.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Paris 2024, Tony Estanguet amesema kwamba Michezo ya Olimpiki mwakani itakuwa mfano mpya wa kipekee katika kuandaa michezo ya aina hiyo duniani kote.
Estanguet alinukuliwa na BBC akisema kwamba Paris inataka kuwa mfano wa sehemu nyingine duniani katika kuandaa Michezo ya Olimpiki katika namna ambayo mazingira yatalindwa.
“Tunataka kudhihirisha kwamba Paris na Ufaransa wanaweza kuwa wenyeji wa michezo ambayo itakuwa katika namna tofauti na ambavyo imekuwa ikifanyika siku za nyuma” alisema Estanguet katika mazungumzo yake na BBC.
Michezo ya Olimiki itafanyika kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11 mwakani katika jiji la Paris na kufuatiwa na Michezo ya Olimpiki Maalum au Paralympics inayohusisha walemavu wa viungo ambayo itafanyika kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 8.
Moja ya malengo ya waandaji ni kuhakikisha kunakuwa na mpango maalum wenye nia ya kupunguza hewa ukaa kwa asilimia 50 zaidi ya ilivyokuwa katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 na 2016.
Paris hata hivyo wana kazi kubwa ya kufikia malengo hayo hasa baada ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 ambayo ilifanyika mwaka 2021 ambayo iliweka rekodi kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha hewa ukaa.
Tafiti hata hivyo zilionesha kwamba Tokyo walifanikiwa kwa sababu ya ugonjwa wa korona ambao kwanza ulisababisha michezo hiyo kufanyika mwaka 2021 badala ya 2022 lakini pia ugonjwa huo ulisababisha mashabiki na hata washiriki kuwa wachache kutokana na zuio la kusafiri.
Michezo ya Olimpiki ni aina ya tamasha kubwa la michezo duniani linaloongoza duniani kwa kushirikisha michezo na wanamichezo wengi kutoka mataifa karibu yote duniani.
