Na mwandishi wetu
Sare ya mabao 2-2 iliyoipata Simba juzi Jumamosi dhidi ya timu ya KMC haijamfurahisha kocha Abdelhak Benchikha akisema wamepoteza pointi mbili muhimu ambazo zingewaweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Sare hiyo imeifanya Simba isalie kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 23 baada ya kushuka uwanjani mara 10 ikiwa imeshinda michezo saba, sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.
KMC wao wameendelea kusalia kwenye nafasi ya nne kwa pointi zao 21 baada ya kushuka uwanjani mara 14 wakiwa wameshinda michezo mitano sare sita na kufungwa mechi tatu.
Benchikha alisema bado safu yake ya ulinzi imeendelea kupunguza umakini kwenye dakika za mwisho kwani bao walilopata KMC linakuwa la pili kufungwa baada ya lile la Wydad, jambo ambalo halikubaliki kwa wachezaji wakubwa kufanya kosa la aina hiyo.
“Niliongea mapema kabla, kuwa huu ni mchezo mgumu kwani tumetoka kucheza mechi kubwa dhidi ya Wydad lakini pia kipindi cha mapumziko kinakuja hivyo kuna kitu kinapungua.
“Tulifungwa bao kipindi cha kwanza tukafanya masahihisho kwa kusawazisha kipindi cha pili na kufunga bao la kuongoza lakini tukaruhusu bao la kusawazisha na kuvuruga malengo yetu,” alisema Benchikha.
Kocha mkuu wa KMC, Abdihamid Moalin alisema amefurahishwa na wachezaji wake kwa kiwango bora walichokionesha kwani wamepata pointi moja mbele ya timu bora ndani ya nchi hivyo anajivunia walichovuna.
“Tulikuwa na mpango wa kuanzisha mashambulizi kwa kushtukiza kwani tulijua makosa ya safu ya ulinzi ya Simba ndio maana kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi tatu lakini tukashindwa kumalizia.
“Nashukuru kwa tulichopata kwani wakati mwingine mipango inafanikiwa na wakati mwingine haifanikiwi, tunachukua pointi hii moja na kusonga mbele,” alisema Moalin.
