Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa KMC, Waziri Junior aliyefunga mabao yote mawili kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba jana Jumamosi amesema siri kubwa ya kiwango chake ni kuaminiwa na kocha wao Abdiamin Moallin.
Waziri alifunga bao la kuongoza dakika ya 31 kabla ya kufunga bao la kuchomoa dakika ya 88 na kuipa KMC pointi moja kwenye mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
“Unajua kikubwa ni kuwa makini na kazi uwanjani lakini pia kocha amekuwa akinipa mbinu mbalimbali ikiwemo ya kwenye mchezo wa Simba ya kukimbia nyuma ya migongo ya mabeki wa kati na imeonekana nikapata mabao mawili.
“Niseme tu kila kitu ni kocha kwenye kuimarika kwangu msimu huu, maana mwalimu anapokupa nafasi na kukuamnini, unaendelea kupambana, hata ukikosea anakueleza na kukupa nafasi, kwa hiyo siri kubwa ni mwalimu,” alisema Waziri mchezaji wa zamani wa Yanga.
Katika mechi dhidi ya Simba, mabao ya Simba yalifungwa na Saido Ntibazonkiza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 57 na Jean Baleke Baleke kwa kichwa dakika mbili baadaye akimalizia mpira uliopigwa na Shomary Kapombe.
