Na mwandishi wetu
Baada ya kupata ushindi katika mchezo wa kwanza akiwa na Geita Gold, kocha Denis Kitambi amewasifu wachezaji wake kwa walivyojituma, kufuata maelekezo na kuiadhibu Singida Fountain Gate kwa bao 1-0.
Geita ilipata ushindi huo jana Alhamisi ikiwa Uwanja wa Nyankumbu, Geita na kupanda kutoka nafasi ya 13 mpaka nafasi ya 10 ikiwa imejukusanyia pointi 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
“Kwanza niwapongeze vijana wamepambana dakika zote 90 na pia sisi ndio tuliotengeneza nafasi nyingi zaidi, tulipaswa kushinda zaidi ya bao moja lakini kingine kipa amefanya kazi nzuri ametuokoa kutafuta pointi tatu.
“Tangu mwanzo niliwaambia kwamba njia pekee ya kuifunga Singida ni kupiga mipira mingi kutokea pembeni na kweli tumepata bao kwa njia hiyo, kwa hiyo pongezi tena kwao kwa kufuata maelekezo na pia wameonesha kujituma mno, na nadhani huu ni mwanzo mzuri, tuzidi kushikilia hapa,” alisema Kitambi.
Kitambi ambaye ametua Geita akitokea Namungo kurithi mikoba ya Hemed Morocco, amesema kuwa ataendelea kuijenga timu hiyo kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye kila mchezo akiwataka vijana wake kujituma zaidi ya wapinzani katika kila mechi iliyo mbele yao.
Kwa matokeo hayo, Singida imeendelea kusalia nafasi ya nne ikiwa na pointi 20 baada ya michezo 14 iliyoshuka uwanjani mpaka sasa.
