Liverpool, England
Nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk ameikana hoja ya Roy Keane kwamba kauli yake kuhusu mechi yao na Man United mwishoni mwa wiki inaonesha jinsi mchezaji huyo alivyo na kiburi.
Akiizungumzia mechi hiyo, Van Dijk alisema kwamba kulikuwa na timu moja tu iliyocheza ikitafuta ushindi, kauli ambayo Keane hakuifurahia na kuitafsiri kuwa ni ya mtu mwenye kiburi.
Keane, nahodha wa zamani wa Man United ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka wa kituo cha televisheni cha Sky alisema kuna kauli ya kiburi iliyotoka kwa mchezaji huyo kwa kuipuuza United kwa kiasi kile.
“Nampenda Roy Keane na kama alisema hivyo ni sawa, amekuwa mtu wa Manchester United kwa wakati wote na naelewa angejibu mapigo kwa namna ile lakini nilijua nilichokisema na hakika sioni kiburi cha aina yoyote,” alisema Van Dijk.
“Kila mtu aliyeangalia ile mechi huenda aliiona hali ile, tulikuwa tukienda mbele, tulipata nafasi na hatukufunga na hilo ni jambo linalokera,” alisema Van Dijk.
Liverpool ilitawala mchezo kwa asilimi 69 na kushambulia mara 34 lakini haikuweza kupata goli dhidi ya Man United ambayo katika mechi hiyo ilitumia zaidi mfumo wa kujihami.
Mechi hiyo iliyopigwa Jumapili ni ya kwanza ya nyumbani kwa Liverpool msimu huu kutoka bila ushindi na matokeo hayo yanaifanya ibaki nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England nyuma ya vinara Arsenal.
