Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki amesema kuwa lengo lake msimu huu ni kuweka rekodi ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora kwenye Ligi Kuu NBC.
Aziz Ki aliyetua Yanga msimu uliopita akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast ndiye kinara katika orodha ya wanaoongoza kufunga akiwa amepachika mabao tisa mpaka sasa.
Mchezaji huyo raia wa Burkina Faso alisema malengo yake msimu huu ni kuisaidia Yanga kutetea mataji yake huku pia akili yake ikiwa katika kukisaka kiatu cha ufungaji bora ili aingie kwenye orodha ya wachezaji wa kigeni waliowahi kubeba tuzo hiyo.
“Wakati nakuja hapa (Tanzania) ndoto yangu ilikuwa ni kuisaidia timu yangu kushinda makombe, lakini pia kiu yangu ilikuwa kuwa mfungaji katika ligi jambo ambalo nataka kulifanikisha msimu huu kama nitakuwa fiti.
“Msimu huu umeanza vizuri, malengo yangu ni kuona kwamba ninaweza kuchukua kiatu cha ufungaji na inawezekana kama tutaendelea kupeana ushirikiano na wachezaji wenzangu na pia mwalimu amekuwa akinitaka kufanya mazoezi kwa nguvu na kuongeza umakini kwenye eneo la mwisho,” alisema Aziz Ki.
Aziz Ki ambaye msimu uliopita alifunga mabao tisa, msimu huu ameanza vyema kampeni yake hiyo baada ya kufunga idadi hiyo ya mabao katika michezo 10 hadi sasa.
Wanaomfuatia Aziz katika orodha hiyo ni Maxi Nzengeli wa Yanga na Jean Baleke wa Simba waliofunga mabao saba kila mmoja mpaka sasa.
