Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya Ihefu imeibuka mashindi wa soka wa bonanza la michezo la Misitu ya Sao Hill lililofanyika kuanzia Desemba 9 mwaka huu na kufikia tamati mwishoni mwa wiki kwenye Shamba la Miti la Sao Hill wilayani Mufindi.
Katika mechi ya soka ya kufunga Bonanza hilo ambayo ilivuta hisia za mashabiki wengi, vinara Ihefu waliibwaga Mgololo Misitu kwa penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida.
Kwa ushindi huo, Ihefu wanakuwa wametetea vyema taji hilo ambalo pia walilibeba katika mashindano hayo kwa msimu uliopita.
Mbali na soka, Bonanza hilo pia lilishirikisha michezo mbalimbali ikiwamo kuvuta kamba, kukimbia kwenye magunia, kucheza draft na bao, riadha mbio ndefu na fupi, mpira wa wavu na netiboli na washindi kupewa zawadi mbalimbali.
Bonanza hilo la kila mwaka na ambalo linafanyika kwa mara ya tisa sasa kwenye shamba la misitu la Sao Hill, lengo lake ni kuhimiza upandaji miti na kuimarisha ujirani mwema.
Bonanza hilo limeendelea kuwa mfano halisi wa kutumia michezo na burudani kuhamasisha upandaji miti, kauli mbiu yake inasema: ‘Panda miti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.’
GreenSports Ihefu kinara Sao Hill Bonanza 2023
Ihefu kinara Sao Hill Bonanza 2023
Read also
