Na mwandishi wetu
Yanga imezidi kuiongezea machungu Mtibwa Sugar inayojikongoja kwenye Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa mabao 4-1 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo Stephane Aziz Ki ameonesha umahiri wake baada ya kufunga mabao mawili, la kwanza katika dakika ya 45 ya mchezo huo kwa mkwaju wa penalti. Aziz Ki aliongeza bao la pili dakika ya 66 akiituma pasi ya Kibwana Shomari.
Mabao mengine yalifungwa na Kennedy Musonda dakika ya 76 na Skudu Makudubela dakika ya 83 na bao pekee la Mtibwa lilifungwa na Seif Karihe dakika ya 90.
Kwa Aziz Ki, mabao hayo yanazidi kumfanya aibue ushindani katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu NBC akiwa tayari ametupia wavuni mabao tisa.
Wafungaji wengine wenye mabao mengi kwenye ligi hiyo ni Feisal Salum au Fei Toto wa Azam FC mwenye mabao saba sawa na Maxi Nzengeli wa Yanga na Jean Baleke wa Simba.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 27 ikiwa katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Azam wanaoshika usukani ingawa Azam wana michezo miwili zaidi ya Yanga.
Kwa Mtibwa kipigo hicho kinazidi kuiweka pagumu timu hiyo kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiendelea kuburuza mkia ikiwa na pointi tano pekee katika mechi 13.
Hivi karibuni kocha wa timu hiyo, Zubeir Katwila aliahidi kuwasilisha ombi la kusajili wachezaji wa kuiimarisha timu wakati huu wa usajili wa dirisha dogo.
Soka Yanga yaongeza machungu Mtibwa Sugar
Yanga yaongeza machungu Mtibwa Sugar
Read also
