London, England
Nahodha wa timu ya Luton Town, Tom Lockyer (pichani) ambaye alianguka uwanjani baada ya kupata matatizo ya moyo wakati wa mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth anaendelea vizuri.
Tukio hilo lililosababisha kusimama kwa mechi hiyo lilitokea jana ambapo mechi hiyo iliahirishwa kabla ya klabu yake kutoa taarifa baadaye ikieleza kuwa mchezaji huyo yuko katika hali nzuri.
Wachezaji wote walitakiwa kutoka uwanjani baada ya tukio hilo lililotokea wakati timu zikiwa katika kipindi cha pili na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kubebwa na kuwahishwa hospitali.
Klabu yake iliwashukuru watoa huduma ya kwanza na kufafanua kwamba mchezaji huyo hayuko katika hali mbaya ingawa aliendelewa kufanyiwa vipimo zaidi vya afya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Tom alihamishiwa hospitali, tunachoweza kuwahakikishia mashabiki ni kwamba yuko katika hali nzuri na kwa sasa anafanyiwa vipimo zaidi akiwa kitandani amezungukwa kwa karibu na watu wa familia yake,” ilieleza taarifa ya klabu ya Luton.

Hii si mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kuanguka uwanjani, mwezi Mei alijikuta katika hali hiyo na kuwahishwa hospitali wakati wa mechi dhidi ya Coventry na aliwahi kufanyiwa upasuaji wa moyo na kuelezwa kuwa yuko katika hali nzuri na akaruhusiwa kuendelea kucheza soka.
Uongozi wa klabu ya Luton ambao walikuwa ugenini katika mechi hiyo, umewataka wachezaji, mashabiki na maofisa wao kuwa pamoja na kumpa ushirikiano Tom na familia yake.
Nao uongozi wa klabu ya Bournemouth katika taarifa yao walisema kwamba wapo pamoja na Tom na familia yake na wamefarijika kusikia kwamba anaendelea vizuri.
