Na mwandishi wetu
Kocha wa makipa Tabora United, Razack Siwa amemtabiria makubwa msimu huu kipa wa timu hiyo, John Noble kutokana na kiwango anachoonesha, akiongoza pia kumaliza mechi nyingi bila kuruhusu bao mpaka sasa.
Noble ambaye amesajiliwa Tabora mwanzoni mwa msimu huu akitokea Enyimba ya kwao Nigeria anaongoza kwenye orodha ya ‘clean sheet’ akiwa nazo tano akiwazidi Lay Matampi wa Coastal Union na Djigui Diarra wa Yanga wenye nne kila mmoja.
Akizungumza na GreenSports leo Ijumaa, Siwa raia wa Kenya alisema anafurahishwa na kazi inayofanywa na Noble na hiyo inatokana na kipaji alichonacho na namna anavyosikiliza maelekezo huku akijituma kila kukicha.
“Ni kipa mzuri, ndio maana haishangazi sana kuona anaongoza kwa ‘clean sheets’ maana ana kipaji, anajituma na anasikiliza maelekezo. Najivunia kuwa na kipa kama huyu ambaye pia anatoa changamoto nzuri kwa makipa wenzie waliopo hapa.
“Naamini atafanikiwa zaidi ya hapa, pengine anaweza kuondoka na taji au tuzo yoyote mwisho wa msimu kutokana na kazi kubwa anayoifanya hapa kwa ajili ya timu nzima kwa ujumla,” alisema Siwa.
Noble ambaye awali alikuwa akitajwa kuwaniwa na Simba, aliamua kutua Tabora baada ya kuitumikia Enyimba kwa misimu mitatu huku msimu uliopita akisaidia kuipa taji la Ligi Kuu Nigeria au NPFL.
