Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga SC umeeleza kuwa uko kwenye mikakati kabambe kuhakikisha wanavuna pointi zote sita za mechi zao mbili mfululizo za nyumbani za Ligi ya Mabingwa Afrika ili kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Yanga inatarajia kuumana na Medeama Desemba 20, mwaka huu kisha kuivaa RC Belouizdad Februari 23, mwakani ambapo mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Yanga, Ali Kamwe alisema leo Jumanne kuwa pamoja na mchezo muhimu dhidi ya Mtibwa Sugar ulio mbele yao lakini wanafahamu umuhimu wa alama hizo sita ndio maana wameanza mikakati mapema kuhakikisha wanautumia vyema uwanja wa nyumbani na kutinga hatua inayofuata.
Mpaka sasa Yanga inaburuza mkia kwenye Kundi D ikiwa na pointi mbili baada ya kufungwa na Belouizdad mabao 3-0 kisha kutoa sare inayofanana ya bao 1-1 kwenye mechi mbili dhidi ya Al Ahly na Medeama.
Al Ahly ndiyo inayoongoza kundi hilo kwa pointi tano, Belouizdad ni ya pili kwa pointi nne sawa na Medeama iliyopo nafasi ya tatu.
“Kocha wetu Gamondi (Miguel) anaandaa program itakayotuvusha salama mwezi Desemba na pia mashabiki wajue hatufanyi maandalizi ya timu moja, ni kwa ajili ya kuelekea mwaka mpya pia.
“Mbali na Mtibwa, Desemba 20 tutacheza na Madeama, kwao tulipata pointi moja, hapa Dar es Salaam wanapaswa kuacha alama tatu kisha itakuwa dhidi ya Belouizdad, imekuwa bahati kwetu kucheza mechi mbili za maamuzi kwenye ardhi yetu, nimefurahi hata mashabiki wa Yanga wanafahamu kwa hesabu ya ushindi wa mechi tutakuwa tumeenda robo fainali, hivyo tuko pamoja katika mikakati hii,” alisema Kamwe.
Kamwe alifafanua kuwa anafahamu ratiba ya Desemba kwao imekuwa na mechi nyingi lakini wanajipanga kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na wanarejea kwenye utawala wao kuanzia kwenye ligi kuu mpaka Ligi ya Mabingwa.
Katika ligi, Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 24 baada ya mechi tisa dhidi ya kinara Azam yenye pointi 28 baada ya michezo 12.
