Marrakesh, Morocco
Mshambuliaji wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria, Victor Osimhen ameibuka kinara wa uzo ya mwanasoka bora wa Afrika 2023 akiwabwaga Mohamed Salah wa Misri na Achraf Hakimi wa Morocco.
Osimhen ambaye alikabidhiwa tuzo hiyo jana Jumatatu na rais wa CAF, Patrice Motsepe, anakuwa mchezaji wa kwanza wa timu ya taifa ya Nigeria au Super Eagles, kubeba tuzo hiyo tangu Nwankwo Kanu afanye hivyo mwaka 1999.
Nigeria pia imetamba wanawake ambapo mchezaji wa timu hiyo maarufu Super Falcons, Asisat Oshoala ambaye pia anaichezea timu ya wanawake ya Barcelona, ameendelea kuitetea tuzo hiyo akiwa ameweka rekodi kwa kuibeba kwa mara ya sita.
Kwa mafanikio ambayo ameyapata kwa msimu wa 2022-23, Osimhen alikuwa akipewa nafasi kubwa kubeba tuzo hiyo na haikushangaza kuwabwaga Salah, nyota wa Liverpool na Hakimi wa PSG .
Katika msimu huo, Osimhen mwenye umri wa miaka 24, ameifungia Napoli ya Italia mabao 26 katika mechi 32 na kuiwezesha kubeba taji la Serie A ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo baada ya miaka 33 huku mchezaji huyo akiibuka mfungaji bora.
Kwa Osimhen, tuzo hiyo ni mwendelezo wa mafanikio yake ya msimu uliopita ambapo pia alibeba tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Chama cha Wanasoka Italia aliyoipata mapema mwezi huu.
Osimhen pia ni mchezaji wa kwanza kutoka Nigeria kuingia katika 10 bora ya kuwania tuzo za Ballon d’Or na kushika nafasi ya nane katika tuzo hiyo iliyobebwa na Lionel Messi wa Argentina.

Kwenye timu ya taifa ya Nigeria, aliifungia mabao matano katika mechi nne za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) na tayari Nigeria imefuzu kushiriki fainali hizo zitakazopigwa mwakani nchini Ivory Coast.
Kwa upande wa Asisat, 29, ambaye pia alikuwa na timu ya Nigeria kwenye fainali za Kombe la Dunia la Wanawake nchini Australia na New Zealand mwaka huu, amewabwaga Thembi Kgatlana wa Afrika Kusini na Barbra Banda anayeichezea Shanghai Sengli.
Kwa upande wa makocha tuzo ya wanawake imekwenda kwa kocha wa Afrika Kusini, Desiree Ellis wakati kwa wanaume mshindi ni Walid Regragui wa Morocco ambaye ana rekodi ya kuiwezesha nchi hiyo kuwa taifa la kwanza la Afrika kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.

Mafanikio hayo ya Morocco pia yamembeba kipa wa timu hiyo, Yassine Bounou ambaye ametwaa tuzo ya kipa bora kwa wanaume kama ilivyo kwa kipa wa Super Falcons, Chiamaka Nnadozie aliyebeba tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.
Katika klabu bora, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imebeba tuzo hiyo kwa wanawake wakati Al Ahly ya Misri, timu yenye rekodi ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara 11, imebeba tuzo hiyo kwa upande wa wanaume.
Washindi wa tuzo hizo ambao wote walikabidhiwa tuzo zao jana mjini Marrakesh, huchaguliwa na wajumbe wa kamati ya ufundi ya CAF kwa kuwashirikisha waandishi wa habari, makocha wakuu na manahodha wa timu pamoja na klabu shiriki za michuano ya klabu ya Afrika ambazo zimeingia hatua ya makundi.
