Na mwandishi wetu
Michuano ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake inatarajia kuchezwa kwa mara ya kwanza leo Jumamosi ambapo michezo miwili itapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mchezo wa mapema ni saa 9.00 alasiri utakaozikutanisha JKT Queens dhidi ya Fountain Gate Princess na mchezo wa pili utawakutanisha watani wa jadi, Simba Queens dhidi ya Yanga Princess utakaopigwa saa 12.00 jioni.
Washindi wa michezo hii watacheza fainali wakati waliopoteza watacheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo. Mechi zote hizo zitachezwa Desemba 12, mwaka huu.
Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alisema: “Kwanza tunawapongeza TFF kwa kuhakikisha soka la wanawake lianzidi kukua kwa uwepo wa mechi kama hizi.
“Lakini tunaamini mechi haitakuwa rahisi kwa sababu timu zote zimejiandaa vizuri, tulikaa na kujiuliza tulipokosea msimu uliopita na tumeona mapungufu yetu na sasa tunataka kufanya vizuri katika mchezo huu wa Ngao ya Jamii.”
Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Charles Haalubono alisema wamejiandaa vizuri kukabiliana na Simba ambao anaamini ni timu ngumu lakini kikosi chake kipo tayari kwa mchezo.
“Itakuwa mechi ya ushindani, natambua ni mechi kubwa na ‘derby’ lakini tumejipanga vizuri na tunatambua katika historia hatuna matokeo mazuri, hatutaki kuamini hayo kwa sababu wachezaji wangu wako tayari kwa ajili ya kutafuta matokeo mazuri,” alisema Haalubono.
Kocha Mkuu wa JKT Queens, Esther Chabruma alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika, wachezaji wako katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo dhidi ya Fountain Gate Princess.

“Hatutakuwa na mabadiliko yoyote katika kikosi changu cha ushindani, nitawakosa nyota wangu wawili, katika mchezo hakuna kujiamini sana kwa sababu wachezaji wangu wengi walikuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa na tutapambana kupata matokeo mazuri,” alisema Chabruma.
Kocha mkuu wa Fountain Gate Princess, Masoud Juma alisema: “Tunaufahamu ubora wa JKT Queens, mechi ya mwisho walitufunga lakini sasa tumejipanga vizuri na tutaingia katika mchezo huu kwa nidhamu ya hali ya juu kwa sababu ni mechi ya kutafuta ushindi.”
