Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila ameuomba uongozi wa timu hiyo kutenga kiasi kikubwa cha pesa ili kufanya usajili wa nguvu kwenye dirisha dogo.
Dirisha dogo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 16 na litafungwa Januari 15, mwakani ambapo kocha huyo amesisitiza kuwa maingizo mapya ndio tiba pekee itakayoinusuru timu hiyo na janga la kushuka daraja mwishoni mwa msimu huu.
Katwila alisema kinachoisumbua timu yake ni idadi kubwa ya wachezaji wake kukosa uzoefu hivyo kushindwa kuhimili ushindani uliopo kwenye ligi.
“Bado tunayo nafasi ya kurekebisha makosa yetu lakini tunahitaji kuboresha kikosi chetu kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu na ligi ambao kwa sasa tunawakosa,” alisema Katwila.
Kocha huyo alisema ukiacha uzoefu, wachezaji wengi kwenye timu hiyo wana uwezo mkubwa wa kucheza mpira na ndio maana pamoja na kupoteza idadi kubwa ya mechi lakini wamekuwa wakionesha kiwango bora katika mechi zao nyingi.
Alisema yeye bado ana imani kuwa timu hiyo itafanya vizuri na kubaki kwenye ligi kuu, lakini hilo linaweza kutimia endapo watakiboresha kikosi chao katika dirisha dogo.
Mtibwa Sugar inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tano katika michezo 12 ya Ligi Kuu NBC iliyocheza mpaka sasa.
Soka Katwila aomba fungu la kuiokoa Mtibwa
Katwila aomba fungu la kuiokoa Mtibwa
Read also
