Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi ameeleza kuwa miongoni mwa kinachowafanya kuendelea kupata matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu NBC ni kuimarika kwa safu yao ya ulinzi.
Kitambi (pichani) ameieleza hayo GreenSports Jumatatu hii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo uliochezwa Jumapili hii kwenye, Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Huo unakuwa ni ushindi wao wa tatu katika mechi sita za mwisho za Namungo, kati ya mechi hizo wametoka sare mara mbili na kufungwa mara moja.
Katika mechi sita za awali za ligi chini ya kocha Cedric Kaze, Namungo ilipoteza mechi tatu na kutoa sare tatu.
“Kwanza tumepambana kuimarisha safu yetu ya ulinzi, maana kama ikitokea tumeshindwa kufunga basi tusipoteze pointi, hivyo tunaelekea kufanikiwa na sasa tumehamia safu ya ushambuliaji kuhakikisha nako kunakuwa sawa ili timu iwe kamili kimapambano na kutafuta pointi.
“Kingine ni ushindi wetu wa kwanza tulioupata dhidi ya Ihefu hivi karibuni, maana ilikuwa hata tukicheza nyumbani hatuna morali lakini sasa morali imerejea ndio maana tumeshinda tukiwa nyumbani, hivyo bado tunapambana kukaa sawa na tunaamini tunaelekea kuzuri,” alisema Kitambi.
Baada ya ushindi huo wa Jumapili, Namungo sasa imepanda kutoka nafasi ya 12 mpaka nafasi ya nane ikiwa na pointi 14 kibindoni.
LigiKuu Safu ya ulinzi yaibeba Namungo
Safu ya ulinzi yaibeba Namungo
Read also
