London, England
Mpango wa mshambuliaji wa Livepool Mohamed Salah kuuzwa unatajwa kuwa mwanzo wa klabu hiyo kumsajili mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe baadaye majira ya kiangazi.
Kwa kipindi kirefu matajiri wa Saudi Arabia wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kumng’oa Salah katika klabu ya Liverpool lakini kumekuwa na ugumu kwa mabosi wa Liverpool kukubali kufanya biashara.
Vyanzo vya habari Uingereza katika moja ya habari iliyopewa nafasi leo Alhamisi ni kuhusu mpango huo kwa imani kwamba pesa ya maana itapatikana na kuwa sababu ya kumshawishi Mbappe kukubali kubadili maisha.
Wakati habari hiyo ikipewa nafasi, Mbappe mwenyewe tangu kuanza kwa msimu huu hajawa tayari kujishughulishwa na mambo ya usajili, badala yake ameamua kuitumikia timu hiyo kikamilifu.
Kabla ya kuanza msimu huu Mbappe aliingia katika mzozo na mabosi wa PSG ambao walimtaka ama asaini mkataba mpya au aondoke lakini tangu kumalizwa kwa mzozo huo, mchezaji huyo hakuwa tena mwenye kujishughulisha na mambo ya kuihama PSG.

Msimamo huo hata hivyo unaweza kukutana na ukweli kwamba mchezaji huyo ana shauku ya kutafuta changamoto mpya nje ya PSG, timu ambayo amekuwa nayo kwa muda wa kutosha sasa na kuipatia mafanikio.
Mbappe awali alikuwa akiwindwa na Real Madrid lakini kauli ya kocha wa timu hiyo, Carlo Ancelotti kwamba hahitaji tena huduma ya mshambuliaji huyo inaweza kuwa imemfungia milango ya kujiunga na timu hiyo.
Kwa hali hiyo Mbappe katika kutaka changamoto mpya anaweza kwenda klabu nyingine ikiwamo Liverpool hasa itakapotokea Salah ameondoka, mchezaji huyo atakuwa chaguo la kwanza.
