Madrid, Hispania
Kiwango cha soka la kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham kimeendelea kumfurahisha kocha wake, Carlo Ancelotti ambaye amechambua sifa za mchezaji huyo na nyota wa zamani wa timu hiyo, Zinedine Zidane au Zizou.
Ancelotti alitoa uchambuzi huo jana Jumatano mara baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Napoli, mechi ambayo Real Madrid ilitoka na ushindi wa mabao 4-2 huku Bellingham akicheza soka la kuvutia.
Katika mechi hiyo iliyopigwa katika dimba la Santiago Bernabeu, Bellingham ndiye aliyefunga kwa kichwa bao la pili la Real Madrid baada ya Napoli kupata bao la kwanza kupitia Giovanni Simeone na Rodrygo kusawazisha.
Napoli walisawazisha kupitia Frank Zambo na kufanya matokeo kuwa 2-2 lakini Madrid waliongeza bao la tatu lililofungwa na Nico Paz na Bellingham kutoa pasi iliyozaa bao la nne mfungaji akiwa Joselu.
“Ni vigumu kulinganisha vizazi viwili tofauti, ninachokiona ni uwezo wa Bellingham kuingia kwenye boksi, Zidane hakuwa na hilo lakini kuna sifa na hadhi ya kipekee ambayo Zidane alikuwa nayo na Bellingham hana,” alisema Ancelotti alipotakiwa na waandishi kutoa tathmini yake kuhusu Bellingham na Zidane ambaye alikuwa jukwaani akiangalia mechi hiyo.

Ancelotti hata hivyo alisema kwamba kinachotokea sasa ni soka la zama hizi ambalo linahitaji mchezaji mwenye nguvu zinazohitajika kama ilivyo kwa Bellingham, ambaye kwa haraka unaweza kumuona katika sehemu kubwa ya uwanja.
“Anatushangaza kila siku na katika kila mechi, si kwamba anatushangaza sisi tu bali anamshangaza kila mtu, Bellingham ni zawadi ya soka, kocha wake na wachezaji wenzake wanafurahia kuwa naye na mashabiki pia wanafurahia lakini kila mmoja anafurahia kuona mchezaji mwenye sifa zake na mwenye mtazamo chanya,” alisema Ancelotti.
Bellingham hadi sasa amefunga jumla ya mabao 15 katika mechi 16 za Real Madrid, na zaidi ya hilo ana rekodi ya kufunga goli katika kila mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya aliyocheza hadi sasa.
