Na mwandishi wetu
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda ametimiza ahadi yake kwa kuikabidhi Yanga ng’ombe watano kutokana na ushindi wa mabao matano walioutapa katika mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Simba.
Makonda aliahidi kutoa zawadi ya ng’ombe kwa timu ambayo ingeibuka na ushindi kwa idadi yoyote ya mabao katika mchezo uliochezwa Novemba 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhi ng’ombe hao hivi karibuni katika makao makuu ya Yanga, Mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, katibu msaidizi wa Idara hiyo, Shaibu Akwilombe.
Akwilombe akimwakilisha Makonda alisema wametimiza ahadi yao kama walivyoahidi na CCM inasapoti michezo na inamuunga mkono Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Tumekuja hapa kuikabidhi klabu ya Yanga, ng’ombe watano ikiwa ni ahadi ambayo aliitoa mkuu wetu wa idara ya Itikadi na Uenezi, Paul Makonda na baadae tutakwenda Msimbazi kukabidhi ng’ombe mmoja sababu katika mchezo huo matokeo yalikuwa ni 5-1,” alisema Akwilombe.
Alisema CCM itaendelea kutoa hamasa mbalimbali kwenye michezo ili kusaidia jitihada zinazofanywa na serikali katika kuendeleza sekta hiyo pamoja na kuinua vipaji vya vijana wa Tanzania.
Wiki iliyopita shabiki mmoja wa klabu ya Yanga, pia aliikabidhi klabu hiyo ng’ombe watano na uongozi wa kufanya sherehe kubwa kwa kuwaita mashabiki wake kunywa supu na chapati katika makao makuu ya timu hiyo.
