Na mwanadishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amefuta mapumziko ya wachezaji wake, akitaka wafikie kambini ili kutengeneza mpango mkakati wa ushindi katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Desemba 2, mwaka huu Uwanja wa Mkapa dhidi ya Al Ahly.
Hiyo ni baada ya kipigo cha mabao 3-0 katika mchezo wa jana Ijumaa dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi D linaloongozwa na miamba hiyo ya Algeria.
Gamondi alisema haoni sababu ya kuwapa mapumziko wachezaji sababu kuna muda mchache kabla ya kuivaa Al Ahly na anataka kuzitumia siku chache zilizobaki ili kuwapa wachezaji wake mbinu muhimu zitakazowapa ushindi.
“Mechi ya Desemba 2 ni lazima tushinde kama tunataka kwenda hatua inayofuata kwenye mashindano haya, lazima tuwe na mikakati sababu tunakwenda kukutana na timu nyingine kubwa na mabingwa watetezi ndio maana sioni sababu ya kutoa mapumziko kwa wachezaji,” alisema Gamondi.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Belouizdad alisema ulikuwa mzuri lakini makosa madogo ya kupoteza umakini kwa safu yake ya ulinzi ndio ilisababisha wapoteze mchezo huo na kujikuta wakianza mechi za hatua ya makundi vibaya.
Alisema waliutawala mchezo na kutengeneza nafasi nne lakini walishindwa kuzitumia, kwake siyo mbaya sababu walikuwa ugenini anaamini wachezaji wake wamejifunza kitu na mechi zinazofuata watafanya kwa usahihi kila kitu ikiwemo nafasi za mabao watakazozitengeneza.
Kocha huyo pia aliwaomba msamaha mashabiki wao kwa matokeo kuwa tofauti na vile walivyowaahidi lakini amewaomba wasikate tamaa kwani nafasi ya kuvuka hatua ya makundi kwenda robo fainali ni kubwa kulingana na idadi ya mechi zilizosalia.
Kocha Mkuu wa Belouizdad, Marcos Paquetá aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kimbinu zaidi na kufanikiwa kupata ushindi huo ambao umewapa mwanzo mzuri kuelekea mechi zinazofuata za michuano hiyo huku pia akiwapongeza Yanga kwa mchezo mzuri waliouonesha.
“Ushindi tulioupata utatuongezea hamasa ya kufanya vizuri mechi ijayo ambayo tutacheza ugenini dhidi ya Medeama lakini niwapongeze Yanga pamoja na kuwafunga lakini walicheza vizuri na kutupa ushindani wa aina yake kama wataendelea hivyo wanaweza kusumbua,” alisema Paquetá raia wa Brazil.
