Barcelona, Hispania
Ofisi ya waendesha mashtaka nchini Hispania imetaka beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves apewe adhabu ya kifungo cha miaka tisa jela kwa kosa la kubaka na udhalilishaji kijinsia.
Alves, 40, anakabiliwa na mashtaka ya kubaka na udhalilishaji kijinsia akituhumiwa kufanya makosa hayo Desemba mwaka jana kwenye klabu moja ya usiku katika jiji la Barcelona.
Tangu kuibuka tuhuma hizo, Alves alikamatwa na kutiwa ndani Januari mwaka huu na hadi sasa ameendelea kuwa rumande baada ya kunyimwa dhamana licha ya kukana kufanya kosa lolote.
Katika kujitetea kwake, Alves ambaye pia amezichezea klabu mbalimbali barani Ulaya, amekuwa akisisitiza kwamba kama kuna jambo alilifanya basi alikuwa na makubaliano na mwanamke huyo.
Sambamba na adhabu ya miaka tisa jela ambayo imeombwa na ofisi ya waendesha mashtaka, ofisi hiyo pia imetaka mchezaji huyo amlipe fidia ya Pauni 130,5000 mwanamke anayedaiwa kufanyiwa ubakaji.
Hatua ya kumfikisha Alves mahakamani imekuja baada ya mahakama moja ya Barcelona kueleza kuwa upo ushahidi wa kutosha kumfikisha mchezaji huyo mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo bado haijatajwa na Alves ambaye alikuwa akiichezea timu ya Unam ya nchini Mexico, amefutiwa mkataba na timu hiyo mara baada ya tuhuma hizo kuibuka.
Nchini Hispania kosa la kubaka linaingia katika makosa ya udhalilishaji kijinsia na iwapo mhusika atakutwa na hatia anaweza kujikuta akipewa adhabu ya kifungo jela kati ya miaka minne hadi 15.
Kimataifa Wataka Dani Alves afungwe jela miaka tisa
Wataka Dani Alves afungwe jela miaka tisa
Read also
