Manchester, England
Beki wa Man United, Harry Maguire amekubali msamaha alioombwa na mbunge mmoja wa Ghana aliyedhihaki kiwango chake wakati akichangia usimamizi wa uchumi wa Ghana na kuufananisha na uchezaji mbovu wa mchezaji huyo.
Akitumia mtandao wa Twitte au X, Maguire aliandika, “Tuonane Old Trafford,” kauli ambayo inaonesha kuwa mchezaji huyo amekubali yaishe.
Mbunge huyo, Issac Adongo alikuwa akichangia bajeti ya Ghana mwaka jana na kuufananisha usimamizi wa uchumi chini ya makamu rais wa Ghana, Mahamudu Bawumia na kiwango kibovu cha uchezaji cha Maguire.
Juzi Jumanne hata hivyo Adongo alisema kwamba anataka kusahihisha kauli yake hiyo na kumpongeza Maguire kwa namna ambavyo soka lake limebadilika na kuwa mchezaji tegemeo wa Man United.
Mbunge huyo hata hivyo hakubadili msimamo wake kuhusu lawama alizomtupia makamu wa rais kwa usimamizi mbovu wa uchumi.
Akifafanua zaidi mbunge huyo alisema kwamba alitumia mfano wa Maguire aliyekuwa chini ya kiwango msimu wa 2021-2022 ili kufikisha ujumbe wa kutoridhishwa na jinsi uchumi wa Ghana unavyosimamiwa.
“Kiwango cha Harry kilipoanza kuwa bora niliona analazimika kuombwa msamaha, nikiwa ni mpenzi wa soka ni muhimu kutambua mabadiliko yake,” alisema Adongo.
Bawumia kwa sasa ndiye kiongozi wa serikali ya Ghana anayesimamia uchumi wa nchi hiyo ambao unapitia katika kipindi kigumu nchi hiyo ikiandamwa na madeni yanayotokana na mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).
