Na mwandishi wetu
Kocha mpya wa Tanzania Prisons, Hamad Ally (pichani) ameushukuru uongozi wa timu hiyo kwa kumuamini na kumpa jukumu la kukinoa kikosi chao katika Ligi Kuu NBC.
Akizungumza na GreenSports kocha huyo alisema atahakikisha anatumia uzoefu alionao kuipa matokeo mazuri timu hiyo huku akitegemea ushirikiano wa karibu kutoka kwa uongozi wa timu hiyo.
“Naushukuru uongozi wa Tanzania Prisons kwa imani yao kwangu, nchini kuna makocha wengi wenye uzoefu lakini wameniona mimi, nitapambana kuhakikisha siwaangushi kwa kuiondoa nafasi mbaya iliyopo sasa na kuipandisha nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi,” alisema Hamad.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Prisons, Ajabu Adam alisema sababu ya kumchagua Hamad ni kutokana na uzoefu alionao katika kufundisha timu mbalimbali kwenye Ligi Kuu NBC.
“Tunamkaribisha sana Hamad, imani yetu kwake ni kubwa sana, tunaamini atafikia malengo tunayoyakusudia kwa timu yetu kumaliza msimu huu kwenye nafasi za juu, tumejipanga kumpa ushirikiano wa kutosha ikiwemo kusajili wachezaji atakaowahitaji kuanzia dirisha dogo lijalo,” alisema Adam.
Kocha huyo ambaye amekabidhiwa timu hiyo kutoka kwa Fred Minziro aliyetimuliwa, ana kibarua cha kuitoa Prisons nafasi ya 15 kwenye ligi hiyo baada ya kucheza mechi tisa. Kabla ya kutua Prisons kocha Hamad amewahi kuzifundisha KMC na Mbao FC ya Mwanza.
