Rio de Janeiro, Brazil
Kocha wa timu ya taifa ya Argentina aliyeiwezesha timu hiyo kubeba Kombe la Dunia 2022, Lionel Scaloni amesema anafikiria kuachia ngazi baada ya kuwa na timu hiyo kwa miaka mitano sasa.
Scaloni, 45, alitoa kauli hiyo juzi Jumanne baada ya Argentina kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Brazil katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia iliyopigwa Brazil kwenye Uwanja wa Maracana.
Kocha huyo pia ndiye aliyeiwezesha Argentina kubeba taji la Copa America mwaka 2021 kabla ya kuishangaza dunia kwa kubeba taji la dunia mwaka jana katika fainali zilizofanyika Qatar.
“Argentina inahitaji kocha ambaye ana nguvu na ambaye yuko vizuri, nahitaji kuuweka mpira kando na kuwa mtu wa kufanya tafakuri, nina mengi ya kufikiria kwa wakati huu,” alisem Scaloni.
“Si kwamba nasema kwaheri au kinachofanana na hicho lakini nahitaji kufikiria kwani tumefika mbali na kuna mambo yenye utata katika kutuwezesha kuendelea kushinda,” alisema Scaloni.
Scaloni alikabidhiwa majukumu ya kuinoa Argentina Agosti 2018 akichukua nafasi ya Jorge Sampaoli, kabla ya hapo Scaloni alikuwa akiinoa timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Argentina.
Taji la Copa America alilolibeba na timu hiyo mwaka 2021 ni taji kubwa kwa timu ya Argentina katika kipindi cha miaka 28 na baada ya hapo Kombe la Dunia walilobeba mwaka jana likawa taji la tatu kubwa kwa nchi hiyo tangu mwaka 1986.
