Na Hassan Kingu
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka mjadala kuhusu Nestory Irankunda, mchezaji mwenye asili ya Burundi aliyekuza kipaji chake Australia kabla ya kusaini mkataba wa kuichezea Bayern Munich ya Ujerumani.
Irankunda ambaye ndio kwanza ana miaka 17, licha ya kuwa asili yake ni Burundi lakini alizaliwa kwenye kambi ya wakimbizi mkoani Kigoma nchini Tanzania jambo linalowafanya baadhi ya mashabiki wa soka nchini kuamini kuwa mchezaji huyo anatakiwa kuichezea Tanzania.
Wanaoamini hivyo wamefikia hatua ya kuzilaumu mamlaka za soka kwa kutokuwa makini kubaini vipaji na wamejiwa na mtazamo huo baada ya mchezaji huyo kusaini mkataba na Bayern Munich kabla ya hapo hakukuwa na mtazamo huo na sasa wanaona kama timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imemkosa mchezaji mwenye kipaji.
Awali ya yote tukubaliane jambo moja, kama ni timu ya taifa, Irankunda timu yake ni Burundi, si Tanzania na kama atakuwa na nafasi ya kuchagua timu atachagua Burundi au Australia, si Tanzania.
Nasema hivyo kwa sababu mataifa hayo mawili ndiyo kila kitu kwake na si Tanzania apozaliwa kwa bahati mbaya kutokana na matatizo yaliyotokea nchini mwao.
Irankunda si mchezaji wa kwanza kujikuta katika mazingira ya aina hiyo na uchaguzi unakuwa ni taifa la sili au lile lenye nafasi ya kumtangaza au kumfikisha mbali mchezaji kisoka na hapo mara nyingi huwa nchi za Ulaya.
Kwa Irankunda nchi ya asili ni Burundi na kipaji kimekuzwa Australia, hivyo atachagua maeneo hayo mawili, Tanzania kama ipo basi ni ya mwisho lakini kwangu naona haina nafasi yoyote kwa mchezaji huyo.
Solomon Kalou, nyota wa zamani wa Chelsea, baada ya kuibukia Ivory Coast alicheza na kuendeleza zaidi kipaji chake Uholanzi na japo nchi yake ya asili ni Ivory Coast lakini alipambana kwa nguvu nyingi akitaka kuichezea Uholanzi badala ya Ivory Coast.
Kwa Kalou sababu ilikuwa ndogo tu, aliamini Uholanzi kutampaisha, kutampa nafasi ya kucheza Kombe la Dunia, kufikia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, au fainali na hata kubeba kombe jambo ambalo hakuliona kwa Ivory Coast.

Kuna wakati alilipigania suala hilo hadi kwenye vyombo vya sheria nchini Uholanzi, akakataa wito wa Ivory Coast akiamini angecheza Uholanzi lakini Waziri wa Uhamiaji wa Uholanzi wakati huo, Rita Verdonk alipinga suala hilo licha ya aliyekuwa kocha wa Uholanzi Marco van Basten kumtaka.
Kwa Kalou naye pamoja na kuitaka mno Uholanzi lakini alikuwa na chaguo la nchi ya asili ambayo ni Ivory Coast, hakuwa na nchi ya tatu kama baadhi yetu tunavyolazimisha kwa Irankunda.
Jerome Boateng na ndugu yake Prince Boateng wote hawa asili yao na Ghana lakini wamekuzia vipaji vyao vya soka Ujerumani, kwa sababu wanazozijua wao Jerome aliichagua Ujerumani na Prince aliichagua Ghana.
Kwa hao wawili pia utaona fursa mara nyingi zinakuwa mbili, ni ama nchi ya asili au nchi iliyokuza kipaji kama ambavo Irankunda atafanya.
Ukweli ni kwamba mchezaji wa aina hiyo akiwa na kipaji kikubwa cha kumfikisha hadi Ulaya itakuwa vigumu kwake kuiacha Ulaya au nchi yake ya asili na kuchagua nchi ya tatu.
Mifano ni mingi tu yupo pia Mesut Ozil, nchi ya asili ni Uturuki lakini yeye akaamua kuichezea Ujerumani alikokuzia kipaji chake, hakukuwa na chaguo la tatu na hata kama lingekuwapo kwanza angeangalia nchi hizo mbili.
Kama tutazungumzia soka, Australia kuna maana kubwa kwa Irankunda kuliko Tanzania, Australia ndiko alikokuza kipaji chake cha soka na hadi sasa ni mchezaji tegemeo wa klabu ya Adelaide United ya nchini humo ambayo ataachana nayo rasmi Julai mwakani na kuanza maisha mapya na Bayern Munich.
Unamsikiliza shabiki wa soka anavyozungumza ni kama vile huko Australia kipaji chake kilipokuzwa wao hawana timu ya taifa, hawahitaji mchezaji mwenye kipaji au nchi yake ya asili Burundi nao wala hawamhitaji bali Tanzania tu ndio wenye timu ya taifa na wanahitaji mchezaji mwenye kipaji.
Watanzania tunachoweza kufanya ni kukuza vipaji si kudandia treni yaani kusubiri mchezaji aliyekuwa Tanzania kwa bahati mbaya, kisha tukasubiri akapata umaarufu na kuwa juu kwa kusajiliwa na timu kubwa ndipo tunaanza kumdandia na kuanza kulaumiana kwamba tumemkosaje.
