Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo Jumamosi imeanza vizuri mbio za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kuichapa Niger bao 1-0 katika mechi iliyopigwa mjini Marakech, Morocco.
Bao pekee la Stars lilipatikana dakika ya 59 mfungaji akiwa ni Charles M’mombwa ambaye alifumua shuti kali la chini lililombabatiza beki mmoja wa Niger na kumchanganya kipa Mamadou Tanja kabla ya kujaa wavuni.
Timu zote zilionesha uhai wa kushambuliana mara kwa mara ambapo katika dakika ya 36, Niger walimajaribu kipa Manula baada ya Mustapha Hairoo kufumua shuti baada ya kuitoka safu ya ulinzi ya Stars lakini kipa Aishi Manula alikuwa makini na kuudaka mpira huo.
Dakika ya 70, Samatta aliunganishiwa pasi safu na Kibu Denis lakini akiwa yeye na kipa alipiga shuti la chinichini ambalo liliokolewa na kipa huyo kabla ya Samatta akuuwahi mpira huo lakini bado hakuweza kuipa Stars bao.
Dakika mbili baadaye Haji Mnoga akiwa karibu na lango la Niger aliuwahi mpira ulioanzia kwa Novatus Dismas lakini akakosa umakini na kufumua shuti kubwa ambalo lilipaa juu na kutoka nje ya lango la Niger.
Katika dakika tano za mwisho, Niger walilisakama lango la Stars na kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kurudi nyuma kwa lengo la kujihami ambalo Samatta alipewa kadi ya njano kwa kumchezea rafu mchezaji wa Niger aliyekuwa akielekea kwenye lango la Stars.
Stars iliyo Kundi E sasa inasubiri kuumana na Morocco katika mechi itakayopigwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam. Timu nyingine za kundi hilo ni Zambia, Congo Brazaville na Eritrea ambayo hata hivyo imejitoa.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2026, Afrika kwa mara ya kwanza itawakilishwa na jumla ya timu 10 kutoka makundi tisa kwa kila kundi kutoa timu moja na nyingine moja itatoka miongoni mwa timu zitakazoshika nafasi ya pili kwa kucheza play off.
Kombe la Dunia Stars yaichapa Niger 1-0
Stars yaichapa Niger 1-0
Read also
