Na mwandishi wetu
Kocha mpya wa Coastal Union, David Ouma (pichani katikati) ameahidi kuirudisha timu hiyo kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu NBC.
Ouma aliyetangazwa na timu hiyo wiki iliyopita, amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea kwao Kenya alipokuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa, Harambee Stars.
Akizungumza leo Jumanne, kocha huyo alisema kinachompa matumaini ni ubora waliokuwa nao wachezaji wengi wa timu hiyo pamoja na vipaji murua walivyojaaliwa navyo.
“Nimevutiwa na vitu vingi kwa muda mfupi tangu nimejiunga na Coastal, kikubwa ni uwezo waliokuwa nao wachezaji wangu, wengi wana umri mdogo na ni wapambanaji, naamini nikiongeza mbinu zangu tutakuwa miongoni mwa timu zinazopigania ubingwa msimu huu,” alisema Ouma.
Kocha huyo alisema anajua hawapo nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi lakini malengo yake ni kutumia mapumziko ya kalenda ya Fifa kukiimarisha kikosi hicho ili ligi itakapoendelea wapate matokeo mazuri.
Coastal ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikikusanya pointi saba katika michezo tisa iliyocheza hadi sasa, ikiwa imeshinda mchezo mmoja, imefungwa minne na kutoka sare mechi nne pia.
